Skip to main content

Epuka chuki hata dhidi ya maadui kwa maana chuki humchukiza Mungu

Kila kiumbe aliye duniani  au  hata mbinguni anao  au   amewahi  kuwa na maadui kwenye maisha yake. Ndugu yangu msomaji pengine wapo watu ambao unaamini ni maadui zako. Unajua wazi kuwa hawapendi ufanikiwe. Hujaribu kutafuta namna ya kuhakikisha hufikii malengo yako kwenye maisha ama kile alichokupatia Mungu kinapotea. Kama unao watu hawa hakika ni maadui zako.



Unajua la kufanya ndugu  msomaji unayependwa na Mungu? Pambana nao maadui zako lakini kwa njia alizoelekeza Mungu wa mbinguni. Pambana nao kwa upendo kwa maana chuki humchukiza Bwana. Kama adui yako ana njaa mpe chakula; kama ana kiu; mpe kitu anywe maana ukifanya hivyo utampalia mkaa wa moto kichwani pake (Warumi 12:20).

Kupalia mkaa wa moto kichwani kwa adui ina maana ya kutoa ‘adhabu ya kiungu’. Hii ni kwa mujibu wa wanathiolojia wakubwa wa kikristo kama Charles Ellicott, Matthew Henry na Albert Barnes. Mpe adhabu ya kiungu adui yako. Adhabu ya kiungu ni ile itakayomfanya ajutie ama kujiuliza kwa kina juu ya uadui alio nao kwako. Visasi visivyo vya kiungu dhidi ya adui yako haviwezi kumpendeza bwana Mungu wa mbinguni na vitakuletea hasara.

Hapana shaka umewahi kuyasikia maneno ya Yesu aliyowaambia wanafunzi wake siku moja ya sabato. Yesu alisema wapendeni maadui zenu, watendeeni mema wale ambao wanawachukia nyinyi (Luka 6:27). Wabarikieni wale ambao wanawalaani nyinyi, waombeeni wale ambao wanawaonea nyinyi (Luka 6:28).

Akupigaye shavu la kushoto mgeuzie na lingine. Haya mafundisho yote ya Kristo yanaelekeza kupalia kaa la moto kichwani mwa adui. Yaani kutoa adhabu ya kiungu kwa adui yako. Yesu baada ya kusulubishwa msalabani akawaombea msamaha kwa Baba waliomsulubisha. Alitamka ‘Baba wasamehe kwa kuwa hawajui walitendalo’ (Luka 23:34). Na wewe pia uwe na moyo wa namna hiyo dhidi ya maadui zako. Visasi na adhabu za kishetani havifai.    

Ni mangapi na wewe huwa unamkosea Mungu ndugu yangu? Mangapi umefanya ambayo Mungu yamemchukiza lakini bado anaendelea kukupa neema ya kuitumia pumzi yake bure? Mungu hakuoni wewe kama adui pamoja na yote maovu unayofanya. Hivi ndivyo pia inapasa uwatendee wanaokufanyia ubaya kama unahitaji Mungu akufanyie hivyo pia.

Sina shaka umeshawahi kusali kwa Mungu kuwa akusamehe kama ulivyowasamehe waliokukosea kama lisemavyo neno (Mathayo 6:12). Je ni kweli huwa unawasamehe waliokukosea? Kama jibu ni hapana basi nasikitika Mungu pia hatasamehe madhambi ya kwako. Epuka chuki kwa maana chuki humchukiza Mungu.   

Tunashukuru umesoma maneno haya kwa ajili ya bwana Mungu wako. Inakupasa uyafanyie kazi ili uwe karibu na neema za Baba yetu aliye mbinguni. Ukifanya kinyume na mafundisho haya ya Biblia Mungu hatakuwa pamoja na wewe. Share na wengine neno hili la Mungu kama inavyokuelekeza Biblia kwenye Marko 16:15 na Mungu atatimiza haja kuu ya moyo wako hivi karibuni. Amen. 

Kama umeguswa tafadhali changia juhudi zako ili neno la Mungu lisambae zaidi. Bofya >>>HAPA<<< kuchangia na Mungu wa mbinguni atakuinua. Amen.